DHIBITI MAGUGU KATIKA KILIMO CHA ZAO LA ALIZETI

Tanzania ni nchi ya 16 katika uzalishaji wa zao la alizeti duniani. Katika eneo lote linalolimwa Tanzania; asilimia 6 hutumika kwa ajili ya kilimo cha alizeti. Zao hili linatumika kwa matumizi mbalimbali ikiwemo kutengeneza mafuta, kuengeneza bidhaa mbalimbali viwandani mfano rangi na sabuni. Mabaki yanayopatikana baada ya kukamua mafuta (mashudu) hutumika kama chakula kwa ajili ya mifugo kama ng’ombe, mbuzi, nguruwe au sungura.

Zao hili linakabiliwa na changamoto ya magugu hasa katika hatua za mwanzo za ukuaji. Zao la alizeti haliwezi kustahimili magugu na hivyo ni rahisi mkulima kupoteza kiwango kikubwa cha mazao endapo magugu hayatadhibitiwa. Magugu hushindana na alizeti katika mahitaji muhimu kama mwanga wa jua, nafasi, maji, virutubisho kwenye udongo n.k.

Picha: Zao la alizeti

Ili kukabiliana na magugu wakati wa kulima zao la alizeti ni muhimu mkulima afanye yafuatayo:

  1. Maandalizi bora ya shamba..

Hii ni pamoja na kusafisha shamba linalotarajiwa kupandwa mazao. Hakikisha shamba ni safi kabla ya kupanda mazao kwa kulima na kuondoa magugu yote shambani.

  1. Kutumia mzunguko wa mazao.

Kubadilisha aina ya mazao katika shamba ni njia nzuri ya kupunguza uwezekano wa kuwepo kwa magugu shambani. Hii inaweza kufanya kutoka msimu mmoja hadi mwingine. Zao la alizeti linaweza kufanyiwa mzunguko na mazao kama mahindi, mtama au ngano.

  1. Kufanya palizi baada ya kupanda

Ni muhimu kufanya palizi mara kwa mara hasa katika hatua za mwanzo za ukuaji wa alizeti. Ndani ya wiki sita za mwanzo hakikisha palizi imefanyika kikamilifu walau mara mbili kutegemeana na hali ya shamba.

  1. Matumizi ya viuatilifu vya kuua magugu (viuagugu).

Dawa za kuua magugu ambazo hazina madhara kwa alizeti zinaweza kutumika. Dawa hizi zinaweza kutumika kabla ya magugu kuota (Mfano pendimethalin, metolachlor) na pia baada ya magugu kuota mfano atrazine.

  1. Matumizi ya vifaa safi.

Endapo vifaa vinavyotumika shambani mfano jembe na vinginevyo vinatumika katika mashamba mengine pia; ni muhimu visafishwe kabla ya kutumika kwenye shamba la alizeti. Hii itapunguza uwezekano wa kusambaza mbegu za magugu kutoka shamba moja kwenda jingine.

“Mavuno bora hupatikana kwa kuzingatia kanuni zote bora za kilimo; hakikisha unafuata bila kupuuzia hatua yoyote katika kilimo”

Kwa ushauri wa kitaalamu na mahitaji ya pembejeo bora za kilimo ikiwemo mbolea, mbegu, viuatilifu na vifaa vya kuhudumia mazao shambani, karibu sana ofisini kwetu FARM Co Ltd. Tunapatikana mkoa wa Morogoro, mtaa wa Misufini tumepakana na Cherry Hotel.